Alhamisi 13 Agosti 2026 - 02:46
Sira ya Mtume Mtukufu (saww) Ni Kielelezo Kamili cha Rehema, Uadilifu, Maadili na Umoja kwa Wanadamu

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muhammad Hassan Jaafari amesema katika ujumbe wake kwamba: Sira ya Mtume (saww) na Ahlul Bayt (as) haipaswi kuishia katika kuwapenda na kuomboleza tu, bali tunapaswa kuyatekeleza mafundisho yao katika maadili, mwenendo na maisha yetu ya kila siku.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muhammad Hassan Jaafari, Imam wa Swala ya Ijumaa wa Skardu, Baltistan, Pakistan, kwa mnasaba wa kufika siku za mwisho za mwezi Safar na kumbukumbu ya kufariki dunia kwa Mtume Mtukufu wa Uislamu (saww), pamoja na kumbukumbu ya kuuawa kishahidi Imam Hassan al-Mujtaba (as) na Imam Ridha (as), ametoa salamu za rambirambi katika siku hizi za majonzi kwa Imam wa Zama (aj), Mara'jii wakubwa, wanazuoni na Waislamu wote, hususan wapenzi wa Ahlul Bayt (as).

Akizungumzia nafasi na daraja tukufu la Mtume Mtukufu (sawe), amesema: Maisha mema ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) ni kielelezo kamili kwa wanadamu katika rehema, uadilifu, maadili na umoja, na mafundisho ya Mtukufu huyo yanaweza kuwa mwongozo kwa jamii za Kiislamu katika njia ya maendeleo na mshikamano.

Mwanazuoni huyo mashuhuri wa Pakistani ameongeza kwamba: Imam Hassan al-Mujtaba (as) pia, kwa subira, uvumilivu na mtazamo wa mbali, daima aliweka maslahi ya Umma wa Kiislamu mbele, na kwa kutekeleza jukumu lisilo na mfano, aliilinda heshima ya Uislamu na maslahi ya Waislamu.

Amesisitiza kwamba: Leo hii, wajibu wetu ni kutouwekea mipaka mwenendo wa Mtume Mtukufu (saww) na mafundisho ya Ahlul Bayt (as) katika kuonesha mapenzi na kuandaa sherehe na maadhimisho pekee, bali tunapaswa kutekeleza kwa vitendo mafundisho hayo katika mwenendo wetu, mahusiano ya kijamii, miamala na maisha yetu ya kila siku.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muhammad Hassan Jaafari, mwishoni mwa ujumbe wake, alimuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awajaalie Waislamu wasimame imara katika njia ya kuufuata mwenendo wa Mtume Mtukufu (saww) na mafundisho ya Ahlul Bayt (as), na awajaalie wote tawfiki ya kuyatekeleza mafundisho ya watu hao watukufu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha